Tarehe 17 Machi, 2010, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete alitia saini Muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi na hivyo Muswada huo kuwa Sheria Kamili. Muswada huo ulipitishwa tarehe 11 Machi 2010 katika Mkutano wa 18 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivi karibuni, Mheshimiwa Dk Wilbrod Slaa alitoa madai kwamba kuna kifungu kidogo cha (3) ambacho kimeingizwa katika kifungu cha 7 cha Sheria hiyo isivyo halali au “kinyemela”. Kifungu kidogo cha 7(3) kinaweka masharti yanayohitaji uthibitisho wa wajumbe wanaounda Timu za Kampeni za Wagombea wa Kiti cha Urais, Ubunge na Udiwani. Mheshimiwa Dk. Slaa anadai kwamba kifungu cha 7(3) hakikuwepo kabisa kwenye Muswada wa Sheria uliojadiliwa na hatimaye kupitishwa na Bunge.
Kwa kuzingatia madai ya Mheshimiwa Dk. Slaa, Vyombo vya Habari vimekuwa vikitoa maelezo mbalimbali kuhusu suala hili. Katika mazingira haya, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatoa Taarifa kwa Umma yenye lengo la kufafanua kile kilichotokea Bungeni hususan uandishi wa kifungu cha 7(3) katika Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
Kutokana na marekebisho yaliyopendekezwa na Wadau na Wabunge, Bunge liliagiza Muswada uchapishwe kwa mara ya pili. Baada ya Muswada huo kuchapishwa kwa mara ya pili, kifungu cha 7 hakikuwa na vifungu vya (1), (2) na (3). Hata hivyo, kwa kuzingatia hoja zaidi zilizotolewa na Wabunge kuhusu makundi ya Sanaa na Viongozi wa Vyama wanaoweza kumsaidia Mgombea wakati wa Kampeni za Uchaguzi, Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu wa Bunge) Mhe. Philip S.Marmo, iliandaa Jedwali la Marekebisho ambalo lilifanya marekebisho katika kifungu cha 7.
Marekebisho hayo ni:
(a) kukitaja kifungu cha 7 kilichokuwepo kuwa kifungu kidogo cha (1) katika kifungu hicho hicho cha 7.
(b) kuongeza kifungu kidogo cha (2) ili kuongeza makundi ya sanaa na kundi la watu wanaoweza kufadhiliwa na Mgombea kwa chakula, vinywaji, malazi na usafiri wakati wa Kampeni za Uchaguzi.
Kwa kuwa uamuzi huu ulifanyika wakati wa Kamati ya Bunge Zima, Mwenyekiti aliagiza kwamba suala hilo la kuweka marekebisho hayo, lizingatiwe wakati wa kutoa tafsiri ya maneno “timu ya kampeni”. Kwa kuzingatia mapendekezo ya Mhe. William H. Shellukindo kwamba idadi ya timu ya kampeni itazamwe na iwekwe wazi badala ya kuiacha wazi tu. Katika kutekeleza hayo, kifungu kidogo cha (3) kiliongezwa kwenye kifungu cha 7 cha Muswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ambapo tafsiri ya msamiati “Timu ya Kampeni” iliwekwa katika kifungu ambacho msamiati huo umetumika. Hii ndiyo sababu kifungu kidogo cha (3) kiliongezwa.
Kwa kuzingatia taaluma ya uandishi wa sheria ilibidi kuongeza masharti yenye amri ya kisheria (Legislative rules) katika kifungu hicho ili tafsiri ya “Timu ya Kampeni” ijitosheleze. Masharti hayo ni yale yanayohitaji uthibitisho wa watu waliomo katika “Timu ya Kampeni”. Kwa maelezo haya ni dhahiri kuwa, kifungu cha 7 kilirekebishwa na kupitishwa na Bunge.
Huu ni utaratibu uliozoeleka wa kutekeleza maelekezo ya Bunge katika Mazingira ambayo Bunge linakaa kama Kamati ya Bunge Zima. Katika hatua hii, Wabunge wanaweza, kupitia Kanuni ya 86(II) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, kupendekeza mabadiliko katika Muswada. Endapo Waziri ataafiki mapendekezo ya Mbunge yeyote,atamjulisha Mwenyekiti na Mwenyekiti akiridhia atamuelekeza Mbunge aliyetoa mapendekezo asome maelezo anayotaka yaingizwe kwenye Muswada. Ikiwa Mbunge aliyependekeza marekebisho hayo hana maelezo mahsusi, Mwenyekiti atamuagiza Katibu wa Bunge ashirikiane na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuweka maneno au Kifungu kinachoweka masharti yenye maudhui aliyopendekeza Mbunge. Mwenyekiti atawahoji Wabunge kama mapendekezo yakubaliwe au la, wakikubali basi waandishi watakwenda kuandika kifungu kwa namna ambayo inatafsiri nia na uamuzi wa Bunge.
Kwa kuzingatia maelezo haya kuhusu hoja za Wabunge ninaridhika kuwa kifungu cha 7(3) cha Sheria ya Uchaguzi kimezingatia matakwa na maagizo ya Bunge sawa sawa. Kifungu hicho hakikuingizwa kwenye Sheria “kinyemela” au kwa hila. Aidha, mtiririko wa mamlaka za kuthibitisha Timu ya kampeni una mantiki sahihi yenye lengo zuri la kufanikisha shughuli za uchaguzi kwa ufanisi.
Imetolewa na
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
29 Machi, 2010
Read more...